Serikali bado inaendeleza harakati za kupambana na ulanguzi wa dawa za kulevya pamoja na uuzaji wa pombe haramu.
Akihutubia wanahabari siku ya Jumamosi, waziri wa usalama wa ndani Joseph Nkaissery alisema kuwa kwa sasa hatua kubwa imepigwa katika vita vya kukabiliana na tatizo hilo.
Nkaissery alieleza kuwa idara ya usalama bado haijalemaza shughuli zake katika harakati hiyo, hasa baada ya rais Uhuru Kenyatta mwezi Agosti, 2015 kuagiza kuanzishwa kwa oparesheni za kuwasaka walanguzi wakuu wa mihadarati katika ukanda wa Pwani baada ya oparesheni dhidi ya pombe kufanyika katika eneo la kati na kuleta natija kubwa kwa wakazi wa eneo hilo.
Nao wanaharakati wa kupambana na utumizi wa dawa za kulevya katika ukanda wa Pwani kwa muda wamekuwa wakitoa shinikizo zaidi kwa serikali kuongeza juhudi zake katika kupambana na suala la ulanguzi wa mihadarati linaloonekana kukita mizizi katika eneo hili.