Wanafunzi pamoja na viongozi wa chuo kikuu cha anuwahi cha Mombasa wameapa kupinga uamuzi wowote wa adhabu watakaopewa na kamati kuu ya chuo hicho inayosimamia nidhamu.
Kupitia kwa kiongozi wa wanafunzi katika chuo hicho Desmond Ocharo, tayari viongozi wote na baadhi ya viranja wameshatoa mtazamo wao mbele ya kamati hiyo ya nidhamu mapema wiki hii, na bado wanangoja hatua na adhabu watachukuliwa na chuo hicho.
Ocharo, kwenye mahojiano na mwanahabari huyu, alidokeza japo kwa fununu, kuwa amepewa marufuku ya miaka mitatu na kuongeza kuwa wenzake vile vile wamepewa kila mmoja marufuku ya mwaka mmoja, lakini akatoa matumaini kuwa hilo halitamtia tumbojoto kwa kuwa ana nafasi ya kuenda mbele ya mamlaka husika na kukata rufaa ili uamuzi huo ubatilishwe.
Aliwataka wanafunzi walioathirika kuwa na subira, na kuwahimiza kuweka rufaa kuhusiana na adhabu watakayopewa na usimamizi wa chuo hicho.
Aidha, alisisitiza kuwa hawana kosa lolote kwani viongozi wote walijaribu lile wanaweza kuona kuwa hakuna madhara yoyote yanatekelezwa na wanafunzi.
Ikumbukwe kuwa usimamizi wa chuo hicho unahitajika kuenda mbele ya kamati teule ya bunge la Kaunti ya Mombasa kutoa mwangaza zaidi kuhusiana na maandamano ya wanafunzi hao, ambayo yalishuhudia kuchomwa kwa malori mawili ya kuzoa taka ya Kaunti hiyo ya Mombasa mwishoni mwa mwezi jana.