Share news tips with us here at Hivisasa

Ilibidi maafisa wa polisi kuingilia kati na kutuliza hali baada ya uchaguzi wa shirikisho la kandanda nchini FKF ulioratibiwa kufanyika katika uwanja wa kaunti ya Mombasa kugeuka uwanja wa mafarakano.

Rabsha ilizuka baada ya mirengo mitatu kinzani kushindwa kuafikiana kuhusu idadi ya wajumbe ambao walihitajika kupiga kura.

Hii ni kufuatia hatua ya bodi ya FKF inayosimamia uchaguzi huo kuchapisha majina ya vilabu 12 pekee kinyume na 56, kama inavyodai mirengo hiyo.

Hata hivyo, baada ya mazungmzo ya kina, mirengo hiyo ilikubaliana kuwa wajumbe 56 wote waruhusiwe kupiga kura lakini afisa msimamizi wa FKF Kenneth Kimani alikataa na kushikilia kuwa wajumbe 12 pekee ndio wanaruhusiwa kupiga kura.

Hatua hii iliwafanya wajumbe hao kuzua rabsha hali iliyowalazimu maafisa wa polisi kuingilia kati na kufutilia mbali uchaguzi huo kwa sababu za kiusalama.

Akizungumza muda mchache baada ya mizengwe hiyo, katibu wa FKF tawi la Pwani Kusini Evans Mwachia, alieleza kusikitishwa na namna bodi hiyo ilivyoendesha uchaguzi.

" Lazima kuwepo uwazi na uhuru. Sijafurahishwa hata kidogo na jinsi uchaguzi huu umesimamiwa," alisema.

Kauli ya Mwachia uliungwa mkono na mgombeaji wa kiti cha naibu rais Twaha Mbarak aliyetaka bodi hiyo kuchunguza na kuwachukulia hatua wote waliohusika katika patashika hiyo.

Uchaguzi wa FKF katika matawi madogo uliratibiwa kufanyika kote nchini ijumaa hii huku ya matawi ukiandaliwa Desemba 7 kabla ya urais kufanyika wiki moja baadaye.