Gavana wa Kaunti ya Mombasa Ali Hassan Joho amelezea hofu yake kuwa huenda uchaguzi mdogo wa eneo bunge la Malindi ukaathiri sekta ya utalii Mkoani Pwani kufuatia tofauti kali za kisiasa zinazoshuhudiwa kwa sasa mkoani humo.
Akizungumza mjini Malindi siku ya Jumanne alipoongoza kampeni za kumpigia debe mwaniaji wa chama cha ODM katika uchaguzi huo, Joho alisema kuwa huenda watalii wakaogopa kuzuru Pwani kipindi hiki ambapo siasa zinaonekana kupamba moto.
"Jameni hizi siasa tunapiga kila siku zitafanya wageni waogope kututembelea, naomba hata kama ni kutofautiana tusizue vurugu, tueneze amani,’’ alisema Joho.
Aidha, Joho aliwahimiza wakazi wa Malindi kumpigia kura mwaniaji wa ODM Willy Baraka Mtengo katika uchaguzi huo, huku akimtaja kama mtu wa pekee anayeweza kuliziba pengo lililowachwa wazi na Dan Kazungu aliyeteuliwa waziri wa madini.
Uchaguzi mdogo wa eneo bunge la Malindi umeratibiwa kufanyika Machi 7, na tayari ushindani mkali umeanza kushuhudiwa baina ya Willy Mtengo wa ODM na Philip Charo wa Jubilee.