Huenda sekta ya utalii nchini na hususan eneo la pwani ikaimarika hata zaidi baada ya kushughudiwa kuwasili kwa meli za kitalii nne katika kipindi cha mienzi miwili katika bandari ya Mombasa.
Hii ni baada ya kuwasili kwa meli ya watalii ya Ms Seven Seas Voyager yenye zaidi ya watalii 1,100 katika bandari ya Mombasa, watazuru sehemu mbalimbali za kitalii ikiwemo kisiwani Mombasa, mbuga za wanyama pori ya Mwaluganje na Shimba hills pamoja na maeneo mengine ya kitalii.
Akiongea na wanahabari katika bandari ya Mombasa siku ya Jumatano baada ya kupokea watalii hao, Meneja mkuu wa shughuli bandarini Mombasa Twalib Khamis amesema kwamba sekta hiyo inatarajiwa kupata meli zingine zaidi ya tano ifikapo mwezi wa pili mwaka ujao.
Wakati uo huo, amesema kwamba kwa ushirikiano na idara za usalama, wadau wa sekta ya utalii na wasimamizi wa bandari hiyo, utalii unatarajiwa kuimarika zaidi na kukuza uchumi wa nchi, huku akisema kwamba juhudi zaidi zaitaimarishwa ili kuboresha sekta hiyo mara dufu.
"Tunatarajia sekta ya utalii kuimarika hata zaidi kufuatia ushirikiano uliopo baina ya idara za usalama, wadau wa sekta ya utalii na bandari ya Mombasa kwa kutuwezesha kupokea meli kubwa zaidi hii ya watalii watakaozuru sehemu mbalimbali na kukuza uchumi wa nchi, na hata kuimarisha biashara ndogo ndogo za kitalii," alisema Khamis.
Kwa upande wake katibu wa shirika la Kenya la Utalii Allan Njoroge, hatua hiyo imeonyesha kuimarika kwa usalama kwani asilimia 60 ya watalii wanataka nchini Marekani, Uingereza na Canada.
Meli hiyo ya watalii iliyotaka nchini Dubai na kuwasili katika bandari ya Mombasa inatarajiwa kuelekea nchini Singapore, Hong kong, kisha baadaye Afrika kusini baada ziara yao ya masaa 12.