Share news tips with us here at Hivisasa

Ufadhili duni umezuilia tume ya ardhi nchini kutekeleza majukumu yake ipasavyo, haya ni kulingana na mwenyekiti wa tume ya mashamba nchini,  NLC Muhammed Swazuri.

Akiongea mjini Nakuru Jumanne katika kikao na maafisa wa sekta ya ardhi kutoka majimbo mbalimbali, Swazuri alisema kuwa katika mwaka wa kifedha wa 2014/2015, tume yao iliitisha shilingi bilioni nane kuendeleza majukumu yake, bali wakaweza kutengewa shilingi bilioni 2 pekee.

Aidha, amesema mwaka wa 2015/2016 kuwa wamepokea shilingi bilioni 1.8, kinyume na iliyoitishwa ya shilingi bilioni 7.2, akidokeza kuwa katika miaka hiyo miwili shilingi bilioni 4 zilinuiwa kuwapa makao wananchi katika maeneo ya Nakuru, Uasin Gishu, Narok miongoni mwa maeneo mengine, hatua ambayo haikuafikiwa.

Wakati uo huo, Swazuri amesema kuwa na mbinu ya kidijitalia ambayo inatumika sasa katika kurahisisha maswala mengi katika sekta hiyo.

“Mashine mpya zinazogharimu shilingi milioni hamsini tayari zimenunuliwa katika kusaidia maswala yanayohusika na mashamba ikiwemo kiasi cha mashamba na ukodishaji wa mashamba katika maeneo mbalimbali,” aliongeza Swazuri.