Do you have a lead on a newsworthy story? Share news tips with us here at Hivisasa!

Wakazi wa eneo la Dekaburey, kaunti ya Garissa wamekuwa wakikabiliwa na uhaba wa maji kwa muda wa majuma matatu kufikia sasa.

Siku ya Alhamisi, wakazi hao waliandamana hadi kwenye ofisi ya shirika la kusambaza maji, GAWASCO, wakilalamikia matatizo ya maji yanayowakumba.

Mwanamume mmoja, Kassim Hassan, ambaye alikuwa akiongoza maanadamano hayo alisema kuwa GAWASCO imetenga na kusahau wakazi wa eneo hilo huku kupata maji safi ya matumizi ikiwa changamoto kubwa sana.

“Tumekuwa na shida ya maji kwa takriban wiki tatu kufikia sasa. GAWASCO imesahau eneo la Dekaburey na ndipo tukaamua siku ya leo kuandamana ili kilio chetu kisikike,” Haji alisema.

Wakazi hao waliitaka serikali ya Garissa kufanya jitihada zaidi kuhakikisha kuwa maji kidogo wanayopata mara kwa mara, yanatibiwa na kuwa salama kwa matumizi

“Tunataka serikali ya kaunti ya Garissa kuhakikisha maji machache tunayopata yametibiwa ili tusipatwe na magonjwa kama vile kipindupindu,” mkazi mmoja alisema.

Kwa upande wake, msimamizi wa GAWASCO, Omar Noor alisema kuwa tatizo la uhaba wa maji limetokana na baadhi ya bomba za kusambaza maji kote kauntini kuharibika.

“Tumekuwa na shida ya uhaba wa maji katika maeneo mengi kwenye kaunti ya Garissa na tatizo ni kuwa baadhi ya mabomba ya kusambaza maji kaunti nzima yameharibika lakini hatulali na tunarekebisha mabomba hayo,’’ Omar alisema.

Wafanyikazi wa shirika hilo walichukua ahadi ya kufuatilia malalamishi ya wakazi hao na tatizo la uhaba wa maji kuzikwa katika kaburi la sahau na kuwasihi watu hao kuwa na subra wakati ambapo matakwa yao yanatimizwa.