Uhaba wa nyanya umeikumba eneo la Rongai kaunti ya Nakuru huku wafanyibiashara waliokuwa wakiuza bidhaa hiyo wakigeukia biashara ya kuuza mboga za kienyeji na vitunguu.
Kwa sasa, mkebe mmoja wa nyanya wa kilo moja unauzwa kwa bei ya shilingi mia moja na hamsini bei ambayo wafanyibiashara wanasema ni ghali mno.
Wakulima waliokuwa wamepanda nyanya katika eneo hilo hasua wanaotoka taarafa ya Noisset, hawakupata mazao mazuri ambayo yanaweza kuwapa faida.
Walisema mimea ya nyanya ilikumbwa na ugonjwa uliopelekea wao kukadiria hasara chungu nzima.
Akizungumza na mwandishi huyu afisa wa kilimo eneo la Rongai Charles Githiri, alisema kuwa afisi yake itafanya uchunguzi ili kubaini ugonjwa uliokumba mmea huo katika eneo hilo ili kupata suluhu la kudumu.
“Tayari tuko katika harakati za kutuma maafisa wetu wa kilimo ili kutadhmini hali katika mashamba mbalimbali ili kuchunguza ni maradhi yapi haswa yaliweza kukumba mmea wa nyanya katika eneo hili la Rongai.” Alisema Bw Githiri katika afisi yake Alhamisi.