Wakazi wa eneo la Kibuyuni katika uwakilishi wadi wa Bofu mtaa wa Likoni wameutaja uhusiano mbaya kati ya mbunge wao na gavana wa Kaunti ya Mombasa kuwa chanzo cha kutohamishwa jaa la kutupwa taka katika eneo hilo.
Wamesema kuwa mbunge wao, Mwalimu Masoud, amekuwa na tofauti za kisisa baina yake na gavana wa Kaunti ya Mombasa Ali Hassan Joho, ambazo zimechangia wao kuendelea kuathiriwa na kudhuriwa na mrundiko wa taka ambao umesababisha kutapakaa kwa uchafu na ufundo mkali wa taka hizo umewasababishia maradhi.
Kwenye mahojiano na wakazi hao siku ya Jumatano katika eneo hilo la taka wakiongozwa na mwenyekiti wa wakazi wa eneo hilo la Kibuyuni, Ali Mwamguno alisema kuwa karatasi za nailoni na uchafu wa aina yote umesambaratishwa na kutapakazwa kila mahali, na hata karatasi zimefunika milango yao.
Mwamguno aliongeza kusema kuwa hata kumetokea maradhi yasiyo ya kawaida kwa watoto wao ambao wanajipata wakitapika kila mara wanapokuwa nyumbani.
“Watoto wetu wanapata maradhi ya kutapika na maradhi ya kuharisha na sharti gavana Ali Joho ajitokeze alitoe jaa hili hapa, na sisi tunamngoja mwaka wa kura,” alisema mwenyekiti huyo.
Baadhi ya wakazi hao pia walisema kuwa magari ya Kaunti ya kuzoa taka hayajawahi kuzoa taka kwa zaidi ya miezi mitatu iliyopita ambapo waliitaka serikali ya Kaunti kuwajibika na kutafuta suluhu la jaa hilo kabla ya kuleta shida.