Halmashauri ya Bandari nchini KPA imekabidhiwa rasmi eneo la kuegesha meli katika Bandari ya Mombasa na wahandishi wa taifa la Japan baada ya shughuli ya ujenzi huo kukamilika rasmi.
Kaimu Mkurungezi wa KPA, Catherine Wairi, amesema kuwa usimamizi wa halmashauri ya bandari wameafikiana kusimamia eneo hilo la 21 hadi pale wawekezaji wa kibinafsi watakapoafikiwa kusimamia eneo hilo.
Kwenye kikao na wanahabari katika afisi za Bandari ya Mombasa huko mjini Mombasa siku ya Jumanne, Wairi alisema kuwa kutokana na mkopa ambao serikali ilichukua kutoka kwa serikali ya Japan na kutia saini mkataba huo, KPA imechukua jukumu la kusimamia eneo hilo ili kukamilisha mkopo huo.
Aidha, alisema kuwa shughuli rasmi za kupakua makasha na kuyasafirikisha katika mataifa mengine inatarajiwa kuanza hivi karibuni baada ya vifaa maalum kukamilishwa kuweka katika eneo hilo.
"Tumepokea eneo hili la 21 la kuegesha meli baada ya kukamilika kwa ujenzi kutoka kwa wahandisi wa taifa la Japan. Kama wasimamizi wa Bandari ya Mombasa, tutasimamia shughuli za bandarini katika eneo hili ili kulipa mkopo ambao serikali ilichukua kutoka kwa serikali ya Japan,” alisema Wairi.
Wakati huo huo, Wairi alisema kuwa Bandari ya Mombasa ni kati ya bandari za kimataifa na kuwa wale wanaodhani ni kati ya raslimali za kaunti wanakosa kufahamu baadhi ya maswala muhimu kwani bandari hiyo ni miongoni mwa raslimali za kitaifa.
Eneo hilo la kuegesha meli linauwezo wa kuhifadhi zaidi ya makasha elfu 500 huku bandari hiyo ikilenga kupokea makasha milioni 2.5 ifikiapo mwishoni mwa mwaka huu.