Ukosefu wa maadili mema katika jamii umetajwa kuwa chanzo kikuu cha watoto chini ya umri wa miaka 18 kujiingiza katika visa vya uhalifu.
Afisa wa Huduma ya jamii katika magereza, Esther Mwalili amesema kuwa suala hilo linafaa kuangaziwa ili kupunguza idadi ya visa vya uhalifu na kuhakikisha kuwa usalama wa eneo la Pwani unaimarishwa.
Akiongea na wanahabari mjini Mombasa siku ya Jumamosi, Mwalili amesema kuwa watoto wengi wanaiga tabia zisizofaa kutoka kwa mazingira duni katika makazi yao yalichangiwa na ukosefu wa maadili mema.
“Tunasikitika kuona vijana wadogo wakijiunga na visa vya uhalifu kutokana na ukosefu wa misingi bora ya maadili mema hatua ambayo inastahili kusuluhishwa ili kuimarisha usalama,” alisema Mwalili.
Ametaja ukosefu wa mwongozo bora wa wazazi, umasikini, mila na desturi zilizopitwa na wakati kuwa chanzo cha watoto kujiingiza katika visa vingine vya uhalifu.
Aidha ametoa mwito kwa wazazi, taasisi za elimu pamoja na viongozi wa kidini kuungana pamoja ili kuwahamasisha vijana na kubadili mfumo wao wa maisha.