Hali duni ya miundo msingi katika shule za umma inachangia matokeo mabaya katika nyingi ya shule hizo, haya ni kulingana na Gavana wa jimbo la Nakuru Kinuthia Mbugua.
Akiongea katika kikao na waalimu wakuu kutoka jimbo hilo mjini Nakuru Jumatano, Mbugua alisema inasikitisha kwani shule nyingi zinakosa mahitaji ya kimsingi kwa masomo yao kama vile maabara na maktaba.
Amesema hali hiyo inawaweka wanafunzi katika ushindani usio sawa, ikizingatiwa shule nyingi za kifahari zina vifaa hivyo.
“Serikali za kaunti zinafaa kushugulikia maswala ya shule za chekechea na vyuo vya Anuai. Lakini serikali yangu itasaidia pia shule za msingi na upili katika kuafikia baadhi ya mambo hayo,” alisema Mbugua.
Hayo yakijiri, Kinuthia alikemea walioteketeza mabweni ya shule ya sekondari ya Mai Mahiu mwishoni mwa mwaka jana.
"Wazazi wanafanya jitihada kujengea watoto wao mabweni, kisha mhalifu anawarudisha nyuma kwa kuyateketeza, ni kitendo cha kulaumiwa, na cha hasara kubwa," alisema Mbugua.