Share news tips with us here at Hivisasa

Wizara ya elimu Kaunti ya Mombasa ikishirikiana na idara ya maji, mazingira na mali asili imeanzisha mpango kwa jina 'Mambo Safi' katika shule za msingi mjini Mombasa.

Akiwahutubia wanahabari katika shule ya msingi ya Sparki siku ya Jumamosi, kaimu waziri katika wizara ya mazingira aliye pia waziri wa elimu kaunti ya Mombasa Lewa Tendai alisema kampeni hiyo inalenga kubadilisha mawazo na fikra za watoto katika kufanya usafi wa mazingira yao.

Ameeleza kwamba mpango huo unanuiwa kuendeleza sera ya Gavana wa Mombasa Ali Hassan Joho iliyobuniwa mwaka 2013 inayolenga kusafisha jiji la Mombasa ambalo kwa muda limetambulika kwa kuzagaa kwa takataka.

Aidha, katibu wa chama cha walimu Knut tawi la Mombasa Dan Aloo pia alihudhuria kampeni hiyo na kuelezea haja ya ushirikiano ili kufanikisha zoezi hilo, huku akisema kuwa wanafunzi wanafaa kukuzwa kufahamu kuwa usafi ni jambo la muhimu na hii itasaidia kutoa ujumbe kwa umma wote Mombasa kuzingatia usafi.

Wakuu wa kaunti watakuwa wakizuru kila shule ya msingi kufanya usafi ikiwa pia ni kutoa uhamaisho.