Usalama umeimarishwa katika Kaunti ya Mombasa hasa maeneo ambayo raia watakuwa wakisherehekea sherehe za mwaka mpya, huku maafisa wa polisi wanaoshika doria wakitakiwa kutowakamata raia wasiokuwa na hatia.
Haya ni kwa mujibu wa Kamishna wa Kaunti ya Mombasa Nelson Marwa alipokuwa akihutubia waandishi wa habari jijini Mombasa siku ya Jumatano.
Hatua hii inajiri baada ya Maafisa wa polisi mjini Mombasa kuwatia mbaroni washukiwa watatu wa uhalifu wakiwa na risasi 56 za bunduki aina ya AK47.
Kulingana na kamanda wa polisi Kaunti ya Mombasa Francis Wanjohi, watatu hao walikamatwa katika hoteli moja ya kukodi maarufu katika eneo la Bondeni, na wakapatikana na vitambulisho vitano vya kitaifa vya watu tofauti.
Jamaa hao wanafanyiwa uchunguzi na maafisa wa kitengo cha kupambana na ugaidi ili kubaini endapo walikuwa na nia yoyote ya kutekeleza visa vya mashambulizi ya kigaidi humu nchini.
Maafisa wa usalama wamekuwa katika hali ya tahadhari zaidi msimu huu wa likizo ya mwisho wa mwaka kufuatia ongezeko la mashmabulizi yanayoendelezwa na wanamgambo wa Al-Shabaab, pamoja na tahadhari iliyotolewa na inspekta generali wa polisi Joseph Boinnet ya kuwataka wananchi kuwa waangalifu zaidi.