Halmashauri ya Bandari nchini KPA imeimarisha usalama wa wawekezaji wanaotumia bandari ya Mombasa kuhakikisha kuwa bidhaa zao ziko salama.
Maneja msimamizi wa bandari hiyo Twalib Khamis amesema kuwa maafisa maalum wa usalama wanashika doria kikamilifu kuhakikisha kuwa ukaguzi wa bidhaa zinazoingia na kutoka ziko salama huku akisema kuwa zaidi ya kamera 250 za CCTV katika eneo hilo zimewekwa.
Akiongea na wanahabari katika bandari hiyo mjini Mombasa siku ya Ijumaa, Khamis amesema kuwa shughuli za uchukuzi, upokeaji na usafirishaji wa mizigo katika bandari hiyo imeimarisha kwa kiwango kikubwa ikilinganishwa na hapo awali.
Amesema kuwa kwa ushirikiano na idara ya usalama nchini, wasimamizi wa bandari hiyo wamepanga mikakati dhabiti ya kuhakikisha kuwa usalama wa bidhaa za wawekezaji na mali ya wananchi unazingatiwa kwa kiwango kikubwa.
"Sisi viongozi wakuu wa Bandari ya Mombasa tumeweka mbinu mbadala kuhakikisha kuwa usalama wa bidhaa za wawekezaji mbalimbali nchini na katika bara la afrika unaimarisha ili kukuza uchumi wa nchini,” alisema Khamis.
Kauli ya meneja huyo imejiri siku chache tu baada ya maafisa wa Halmashauri ya bandari nchini KPA na ile ya KRA kuvamia kampuni ya Auto Port mjini Mombasa na kufunga milango ya kampuni hiyo kufuatia tuhuma za utekelezeji wa bishara za kimagendo.