Share news tips with us here at Hivisasa

Zaidi ya wafanyikazi 2,000 wa kampuni ya kushona nguo ya EPZ iliyoko Changamwe, Mombasa, watalazimika kusubiri kwa mda kabla ya kujua hatima yao, baada ya usimamizi wa kampuni hiyo kukana kuwafuta kazi kama wanavyodai.

Katika mahojiano na kamati ya bunge la Mombasa iliyotwikwa jukumu la kubaini chanzo cha mgogoro huo, wakurugenzi wa kampuni hiyo kupitia wakili wake, siku ya Jumanne walisema kuwa wafanyikazi hao hawakuachishwa kazi bali waliachiliwa baada ya muda wao wa kuhuduma kukamilika.

Kwa mujibu wa wakili huyo, kandarasi ya wafanyikazi hao ilitamatika mwezi Desemba mwaka jana, hivyo hawakuwa na lingine ila kuwaruhusu kuondoka ili kutoa nafasi kwa wengine kuajiriwa.

Hata hivyo, kulingana na mwenyekiti wa kamati hiyo Tom Ogalo, kauli ya wakili huyo inakinzani na malalamishi yaliyowasilishwa na wafanyikazi hao, jambo ambalo lilisababisha pande husika kukosa kuafikiana, na sasa mahojiano hayo yanatarajiwa kuendelea ili kupata suluhu kwa mgogoro huo.

Mapema mwaka huu, takribani wafanyikazi 2,000 wa kampuni ya EPZ iliyoko Changamwe waliandamana wakidai kufungiwa lango la kampuni na kuzuiliwa kuingia, kile walikitaja kama kukandamizwa na mwajiri wao kutokana na hatua yao ya kujisajili na vyama vya kutetea haki za binadamu.