Share news tips with us here at Hivisasa

Uongozi mbaya katika shirika la feri nchini ndio chanzo cha kudorora kwa sekta ya utalii katika eneo la Pwani hasa katika eneo la kusini mwa Pwani, ambalo limeshuhudia idadi ndogo ya watalii kwa sababu ya migogoro inayolikumba shirika hilo.

Hii inajiri siku chache tu baada ya visa vya kufeli kwa feri, jambo ambalo linapelekea kucheleweshwa kwa watalii katika kivuko cha Likoni, ambacho ndicho kiunganisho cha pekee kutoka kisiwani Mombasa kuenda eneo la South Coast.

Kulingana na kiongozi wa muungano wa kushughulikia masuala ya utalii katika eneo la Pwani Monica Solanki, matatizo mengi ambayo yanaendelea kulikumba shirika la hilo la feri yatapata suluhu iwapo mkurugenzi mkuu wa shirika hilo angejiuzulu kwa sababu ya kushindwa kutekeleza wajibu wake ipasavyo.

Akiongea katika ofisi yake jijini Mombasa siku ya Alhamisi, mwenyekiti huyo alisema kuwa sekta ya utalii katika eneo la Pwani inafaa kurekodi idadi kubwa katika msimu kama huu wa likizo ya Desemba, ambapo eneo la Pwani hupokea watalii kutoka maeneo mbali mbali.

Aidha aliongezea kuwa kivuko cha Likoni kimekua kizuizi kikubwa kwa kunawiri kwa sekta ya utalii katika eneo hilo.

Alitoa wito kwa serikali ya taifa kufanya juhudi na kuona kuwa sekta hiyo inalainishwa na kutathmini uongozi wa shirika la feri nchini ili kufaidi nchi kiuchumi.