Share news tips with us here at Hivisasa

Utafiti uliyofanywa na wahudumu wa afya katika hospitali kuu ya ukanda wa pwani umebaini kuwa asilimia 90 ya visa vya ubakaji vinatendewa wasichana wa umri wa chini ya miaka 15 licha ya juhudi za kukabiliana na wabakaji kuidhinishwa.

Kulingana na Afisa wa Afya katika Hospitali kuu ya eneo la Pwani Bi Faiza Ahmed Nassir, visa vya ubakaji vimekithiri kutokana na wazazi wenyewe kutowalinda watoto wao wa kike pamoja na kuwaripoti wahusika kwani wengi wao wanatoka katika jamii moja.

Akihutubia kongamano la akina mama mjini Mombasa siku ya Jumatano katika halfa ya kuadhimisha siku ya dhuluma za wanawake na watoto ulimwenguni, Bi Faiza alisema kwamba katika kipindi cha miezi 11, zaidi ya visa 700 vya ubakaji vimeripotiwa katika hospitali hiyo, huku idadi kubwa ya waathiriwa wakikosa kupata haki zao kwa mujibu wa sheria.

Kulingana na Faiza, maeneo yaliyoripotiwa kukithiri kwa visa vya ubakaji ni Mishomoroni, Likoni, Kongowea, Changamwe na Kisauni katika kaunti ya Mombasa, na kuhimiza mashirika ya kijamii kujitokeza na kupigania haki za waathiriwa ili wahusika kukabiliwa kisheria.

Afisa huyo wa afya amewashutumu baadhi ya wazazi wanaoficha visa hivyo na kuacha watoto wao wakiathirika kiafya na kisaikolojia, huku akisema kwamba lazima wazazi kujitokeza kuwalinda watoto wao na kuripoti visa hivyo kwa wahusika ili sheria zichukuliwe.

"Tunawaomba wazazi kujitokeza na kushrikiana na mashirika ya kijamii pamoja na sisi wahudumu wa afya katika kupigania haki ya mtoto wa kike na mama ili kuwalinda katika dhuluma za kijinsia na ubakaji unaotekelezwa na baadhi ya watu kutoka jamii zetu," alisema afiya huyo.