Share news tips with us here at Hivisasa

Mzozo mpya umeibuka katika shamba la Waitiki lililoko katika eneo bunge la Likoni, Kaunti ya Mombasa baada ya serikali ya kaunti kudai kuwa inamdai mmiliki wa shamba hilo Evanson Waitiki shilingi milioni mia 4 ambazo ni ada ya shamba inayopaswa kulipwa kila mwaka.

Inasemekana kuwa kwa muda wa zaidi ya miaka 20 sasa Waitiki amekuwa akikwepa kulipa ada hiyo kwa serikali zilizopita.

Akizungumza na wanahabari wakati alipozuru shule ya msingi ya Nyali baada ya usimamizi wa shule hiyo kudai kuwa sehemu ya kiwanja chake imenyakuliwa, mkuurgenzi mkuu wa tume ya ardhi nchini Mohammed Swazuri amedokeza kuwa hali hiyo itazingatiwa kuona ni hatua gani mwafaka za kufuatwa katika kukabiliana na madai ya deni hilo.

Hali hiyo imeibua wasiwasi miongoni mwa wakazi wa eneo hilo kwa kile walichokidai kuwa kutofahamu hatima na mwelekeo wa ukaaji wao katika shamba hilo.

Hata hivyo, kulingana na Swazuri, wale wanaoishi katika shamba hilo la Waitiki wanatazamiwa kukabidhiwa hati miliki ya maeneo hayo na rais Uhuru Kenyatta ifikapo siku ya Jumamosi, hatua ambayo inatarajiwa kutatua mzozo wa ardhi hiyo.