Katibu wa chama cha kutetea maslahi ya walimu nchini tawi la Mombasa Dan Aloo ameitaka tume ya kuratibu mshahara wa wafanyikazi wa umma kusitisha zoezi la kuutathmini mshahara wa walimu hadi mbinu itakayotumika katika zoezi hilo iwekwe wazi.
Akizungumza mjini Mombasa siku ya Jumanne, Aloo alisema kuwa utathmini wa mshahara wa walimu utaathiri utendakazi wao kwani tayari wengine wameanza kuhofia kuwa huenda zoezi hilo likasababisha mishahara yao kupunguzwa badala ya kuongezeka.
"SRC lazima ieleze na iweke wazi mbinu itakayotumia katika zoezi la kuutathmini mshahara wa walimu, lazima tujue walimu wetu watahathirika kivipi,’’ alisema Aloo.
Aidha Aloo alidai kuwa hii ni mbinu inayotumiwa na tume ya huduma kwa walimu nchini ili kukwepa kuwapa walimu nyongeza ya mshahara wa kati ya asilimia 50-60 jinsi ilivyoagizwa na mahakama mwaka uliopita.
Kauli ya Aloo inajiri siku moja tu baada ya mwenyekiti wa muungano wa walimu wa shule za upili na vyuo vikuu Kuppet, Amboko Milemba kulikashifu zoezi hilo kwa kile alikitaja kama kuwakandamiza walimu.
Tume ya kuuratibu wa mshahara wa wafanyikazi nchini SRC siku ya Jumanne katika mkahawa mmoja mjini Mombasa ilianza ramsi zoezi la kuutathmini mshahara wa walimu kulingana na masomo yao na masomo wanayofunza.
Picha: Katibu wa chama cha kutetea maslahi ya walimu nchini tawi la Mombasa Dan Aloo pamoja na Wilson Sossion. Aloo ameitaka tume ya kuratibu mshahara wa wafanyikazi wa umma kusitisha zoezi la kuutathmini mshahara wa walimu. Maktaba.