Balozi wa Uturuki nchini Kenya Deniz Eke amesema kwamba nchi yake na Kenya zitashirikiana kwa karibu mno katika kuwakabili magaidi na maharamia ili kuona kwamba usalama wa taifa hili unahimarisha kwa kiwango kikubwa.
Akizungumza mjini Mombasa siku ya Jumanne, Eke alisema kwamba ushirikiano wa mataifa yao mawili utazidi kudumu, huku akisema kwamba wanajeshi wa Kenya watafanya mazoezi pamoja na wale wa Uturuki na kubadilishana mbinu za kuwakabili magaidi ambao ndio tishio kubwa la taifa hili.
Kulingana na Eke, hatua hiyo imeafikiwa baada ya kushuhudiwa msukosuko wa kiusalama baada ya baadhi ya meli kutekwa nyara na maharamia katika bahari hindi ya pwani ya Kenya, huku akisema kwamba hatua hiyo imechangiwa zaidi na muungano wa mataifa ya magharibu yaliyojitokeza kupiga vita ugaidi na uharamia.
Balozi huyo alisistizia ushikamano wa mataifa ya Afrika Mashariki katika kupiga vita ugaidi na uharamia katika mipaka ya nchi zilizopakana na taifa la Somalia linaloaminika kuwa na maharamia wengi zaidi.
"Lazima kwa mataifa ya afrika mashariki kushirikiana kwa karibu mno katika kupiga vita ugaidi na uharamia ndiposa mataifa ya magharibi yatakuwa na ari ya kuunga mkono juhuzi hizo," alisema Eke.
Zaidi ya wanajeshi 240 wa majini kutoka taifa la Uturuki waliwasilia humu nchini kupitia bahari hindi na watakasaidiana na wanajeshi wa majini wa Kenya katika kuimarisha usalama katika bahari hindi ya pwani ya Kenya.