Do you have a lead on a newsworthy story? Share news tips with us here at Hivisasa!

Afisa anayehusika na maswala ya mimea katika eneo la Nakuru Nancy Rotich amedhibitisha kuwa visa vya uwepo wa mbegu bandia nchini vimepungua kwa sasa.

Rotich amesema hatua hii inatokana na uchunguzi wa hali ya juu kuhusiana na uwepo wa mbegu hizo unaofanywa na kampuni ya Kenya Seed pamoja na ile ya KEPHIS (Kenya Plant Health Inspectorate Service)

Hata hivyo, amewataka wakulima kuchukua tahadhari ili kuzuia kuuziwa mbegu bandia huku akiwataka wakulima hao kuweka risiti pamoja na pakiti zilizotumiwa kuweka mbegu hizo kila wanapozinunua na kuzitumia kwa upanzi.

Ni hatua anayosema itawasaidia kila wanapokuwa na tashwishi kuhusiana na mazao yanayotokana na mbegu walizonunua kwani wataweza kupeleka risiti na pakiti hizo kwenye kampuni Kenya Seed ili hatua mwafaka ziweze kuchukuliwa dhidi ya wauzaji wa mbegu hizo.

Isitoshe, amewataka wakulima kutumia nambari ya arafa 20441 iliyozinduliwa mwaka jana na kampuni ya kenya Seed ikishirikiana na ile ya KEPHIS kubaini iwapo mbegu wanazonunua ni bandia ama halali.

Amewashauri wakulima kutuma nambari maalum zinazopatikana kwenye pakiti za mbegu hizo kwa kampuni ya Kenya Seed kupitia kwa nambari hiyo ya arafa na hapo watapata ujumbe unatakaowawezesha kujua iwapo uhalali wa mbegu hizo.