Do you have a lead on a newsworthy story? Share news tips with us here at Hivisasa!

Huku tofauti za maneno kati ya Seneta wa Nakuru James Mungai na Naibu Gavana wa Nakuru Joseph Ruto zikijitokeza kuhusiana na maendeleo ya kaunti, hisia tofauti na hizo zimetolewa na wauzaji wa nguo na matunda mjini Nakuru.

Kulingana na wauzaji wa nguo waliozungumza na mwandishi huyu mjini Nakuru, kwa sasa wameepuka kichapo cha mvua ya El-nino baada ya serikali hiyo ya kaunti kuwajengea maeneo ya kujikinga wakiuza.

Job Mwaniki, anayeuza nguo kwenye kibanda kilicho mkabala na soko la mjini humo alisema kwa sasa hawana tatizo la kuhangaika kufunika bidhaa zao kunaponyesha.

“Mbeleni tuliona kama alikuwa anatufukuza mjini (Gavana Kinuthia), kwa kututoa kwenye barabara za mji, lakini sasa tunaona matunda yake. Wateja wetu walitufuata na sasa wanajua kila mtu anauzia wapi, japo miezi kama miwili hivi hatukuuza vizuri baada ya kuletwa pahali pamoja,” alisema Mwaniki.

Hisia zake ziliungwa mkono na Nancy Mwihaki, muuzaji wa matunda na mboga katika soko la ukulima la Nakuru.

“Hali imerejea kama kawaida, na sasa tunauza zaidi kwa sababu Desemba imekaribia. Lakini katika maeneo mengine kama kwa Rhonda na Kaptembwa wauzaji wanataabika kwa maji ya mafuriko,” aliongeza.

Hata hivyo, changamoto kuu kwa serikali hiyo ni kuhakikisha soko hilo limewekwa mawe ili kupunguzia wanunuzi na wauzaji gadhabu ya matope kunaponyesha.

Mnunuzi wa mboga na matunda Kabon Sogomo, ambaye huuzia viungani mwa mji katika eneo la Kampi ya Moto, alisema ingekuwa kheri kama serikali ya kaunti ingeweka lami ama mawe ili magari yanayoingia kuleta ndizi, machungwa na mboga yaache kuharibu hapa soko kwa matope.

“Mbeleni tungetafuta pahali pa kuweka bidhaa, lakini kwa sasa vibanda hivi vipya vina usalama wa kutosha, hata kama nauza mikufu siogopi kuiacha ndani,” alisema Joyce Kamau.

Seneta Mungai hapo Ijumaa alilaumu serikali hiyo ya kaunti kwa matumizi mabaya ya pesa za mlipa kodi, maneno yaliyokanushwa na naibu gavana Joseph Ruto akimtaka Mungai ‘kuonyesha alichokifanyia kaunti tangu kuchaguliwa’.