Vijana kutoka eneo bunge la Bomachoge Chache kaunti ya Kisii wamelaumu tume ya uchaguzi na mipaka nchini jinsi inafanya usajili wa wapiga kura katika eneo bunge hilo.
Kulingana na vijana hao, baadhi ya wadi katika eneo bunge hilo hazina maafisa wa IEBC ambao wataandikisha wapiga kura, huku wakisema ni njama ya kutoandikisha wapiga kura wa eneo hilo ambao waliapa kutowarudisha viongozi walio mamlakani kwa sasa kwenye viti vyao kwa kukosa kutekeleza na kutimiza ahadi walizotoa.
Wakizungumza siku ya Jumanne katika eneo bunge hilo, vijana hao wakiongozwa na mwenyekiti wao Dennis Kamau na Zachary Bikundo walisema Tume ya IEBC haina uwazi katika uandikishaji wa kura kwa kutofanya usajili katika wadi zingine ambapo inastahili shughuli hiyo kuendeshwa.
“Kuna njama ambayo imepangwa ili tuibigwe kura zetu, wa kwanza tunaolaumu tume ya IEBC kwa kutofanya usajiri katika vituo hivyo tulivyotaja, tunaomba maafisa hao wakuje waandikishe wapige kura mara moja,” alisema Kamau.
Kwa upande wa mwenyekiti wa tume ya IEBC eneo la Nyanza kusini Sarah Ogaro, aliwaomba vijana hao kuwa watulivu na kuahidi maafisa hao kufika sehemu hizo ili kuandikisha wapiga kura.
Ogaro alisema changamoto hizo zimechangiwa kufuatia mashine za usajili huku akiahidi hilo kushughuliwa hivi karibuni.