Kundi la vijana kutoka eneo bunge la Kitutu Masaba limeanzisha kampeni ya hamasisho kwa vijana wanaojihusisha na vitendo vya uharibifu kama njia mojawapo ya kuwasaidia kuepuka tabia hizo. 

Do you have a lead on a newsworthy story? Share news tips with us here at Hivisasa!

Wakiongozwa na mwenyekiti wa kundi hilo Joseph Morumbwa siku ya Jumapili, vijana hao walisema kuwa wamo mbioni kuhakikisha kuwa vijana hao wameasi tabia hizo, na kujihusisha na shughuli zinazoweza kuimarisha maisha yao.

"Tunahitaji kuwafikia vijana wengi ambao hujihusisha na visa vya uharibifu hasa wizi ili kuwasaidia waweze kuwa na uhusiano na jamii kwa kuwa tunahitaji wafanye kazi za kujiendeleza ili waepuke kuadhibiwa, na tunataraji kuwafikia zaidi ya vijana 100 katika eneo bunge lote la kitutu masaba," alisema Morumbwa. 

Morumbwa ameongeza kusema kuwa vijana watakaokubali kuasi tabia zao watasaidiwa kuanzisha biashara, na wale watakaotaka kupata mafunzo ya vyuo vya kiufundi watafadhiliwa kupata masomo. 

"Tutaanza kudadisi uwezo wa wale walio na nia ya kuasi tabia zao na tuko tayari kuwasaidia kufungua biashara huku wale walio na nia ya kujiunga na vyuo vya kiufundi wakipata nafasi ya kujiunga na vyuo hivyo," alisema Morumbwa. 

Ratiba hiyo ya kuwahamasisha vijana itakayochukua wiki tatu inatarajiwa kuanzia kwenye wadi ya Gesima kisha ielekezwe Gachuba, Manga, Rigoma, Kemera na Kisha kumalizia Magombo. 

Muungano huo wa vijana unaongozwa na wakili Victor Swanya.