Baada ya Rais Uhuru Kenyatta kutangaza kuongezwa kwa maafisa zaidi katika kikosi cha polisi nchini, vijana katika eneo la Pwani wameitaka serikali kuhakikisha kuwa hakuna visa vya ufisadi katika zoezi la kusajili makurutu.
Baadhi ya vijana mjini Mombasa wamekashifu jinsi zoezi la kusajili makurutu linavyoendeshwa humu nchini, wakiongeza kuwa mara nyingi hukumbwa na visa vya watu kutoa hongo na kusababisha wengine kukosa nafasi.
Rais Kenyatta siku ya Jumanne alitangaza kuwa idadi ya maafisa wa polisi humu nchini ni ndogo mno kulingana na kiwango cha kimataifa na kusema kuwa idara ya polisi inafaa kuanzisha zoezi la kusajili vijana zaidi kujiunga na kikosi cha polisi nchini.
Wakiongea na mwandishi huyu siku ya Jumatano mjini Mombasa, vijana hao wakiongozwa na Omar Said walisema kuwa vijana wengi hushiriki zoezi hilo mara kadhaa bila mafanikio, licha ya kuwa na vigezo vinavyohitajika.
“Mimi niko sawa lakini nimekosa nafasi mara kadhaa kwani kila nikienda kwenye zoezi la kusajili, wengine wanafaulu kupitia njia za mkato na hapo najipata nimetupwa nje,” alisema Omar.
Omar mwenye umri wa miaka 27 aidha alisema kuwa alifurahishwa na tangazo hilo la rais na kwamba anasubiri zoezi hilo litangazwe rasmi.
Alitoa wito kwa serikali kuhakikisha kuwa inakomesha visa ambapo watu wengi wasiofaa kuingia katika zoezi hilo wanapata nafasi huku wengine wenye vigezo wakiachwa nje.
Rais Kenyatta katika hotuba yake alisema kuwa kunahitajika takriban maafisa elfu 10 ili kuboresha idara hiyo ambayo bado inakumbwa na changamoto.
“Huu mpango unafaa kuanza mara moja na tutahakikisha kwamba tunatimiza mpango wa umoja wa mataifa kuhusu idadi ya maafisa wa polisi wanaohitajika,” alisema Rais Kenyatta.
Kulingana na umoja wa mataifa ni kwamba kwa kila wananchi 400, kunafaa kuwa na polisi mmoja wa kulinda usalama jambo ambalo Rais Kenyatta alikiri kuwa halijatimia humu nchini.