Viongozi wa vijana katika kaunti ya Nakuru wameapa kuwa mstari wa mbele kupigana na ukabila na kutetea nafasi kwenye chama kipya cha Jubilee Party of Kenya.
Wakiongoza na rais wa bunge la vijana katika kaunti ya Nakuru Philip Ngok, vijana hao wamesema kuwa ni jukumu la vijana kusimama kidete na kupigana na ukabila kwa maslahi yao na watu wa Nakuru.
Akiongea na wanahabari, Ngok alisema kuwa ukabila umekuwa kikwazo kwa maendeleo katika kaunti ya Nakuru katika miaka iliyopita na ni wakati wa vijana kumaliza hulka hiyo.
“Sisi kama vijana hatutakaa na kukubali ukabila na siasa za ukabila zitugawanye. Sisi kama viongozi wa vijana tutasimama mstari wa mbele na kuwaongoza vijana wenzetu kuunganisha jamii zote zinazoishi Nakuru,” Ngok alisema.
Ngok aliongeza kuwa kama vijana wataheshimu maoni ya kila kabila katika kaunti ya Nakuru na kusema kuwa kila mkenya anayeishi Nakuru ana haki ya kutafuta nafasi ya uongozi.
“Kila mtu hapa awe mluhyia, kikuyu ama msomali ana haki ya kugombea kiti na wananchi wakimchagua ni sawa kwa sababu Nakuru si ya kabila fulani au fulani bali ni yetu sisi sote,” Ngok alisema.