Wakili Denis Anyoka amewahimiza vijana katika kaunti ya Nyamira kujitokeza kuchukua vitambulisho kutoka afisi za sajili ya vitambulisho katika kaunti ya hiyo.
Akihutubia wanahabari ofisini mwake siku ya Jumamosi, Anyoka alisema kuwa yafaa vijana wajiwasilishe kwenye ofisi za sajili ya vitambulisho ili kuchukua vitambulisho vyao.
"Nimekuwa nikipata ripoti kutoka kwa ofisi za sajili ya vitambulisho kuhusiana na vijana wanaojisajili kupokea vitambulisho kisha wanakosa kuvichukua na ningependa kuwahimiza wajitokeze kuchukua vitambulisho hivyo," alisema Anyoka.
Anyoka aliongeza kwa kuwahimiza wakazi wa kaunti ya Nyamira kutokubali kuwauzia wanasiasa vitambulisho vyao, akihoji kuwa huenda hiyo ikawa ni njama ya wanasiasa kutotaka watu kusajiliwa kama wapiga kura.
"Kuna madai kwamba baadhi ya wanasiasa wananunua vitambulisho kutoka kwa wapiga kura ili kwamba wananchi wasiwe na uwezo wa kupiga kura, na ndio maana nawahimiza wananchi kutokubali kuuza vitambulisho vyao," aliongezea Anyoka.
Picha: Wakili Dennis Anyoka. Amewahimiza wakazi, haswa vijana wa kaunti ya Nyamira kuchukua vitambulisho vyao vilivyo katika afisi kadhaa eneo hilo. WMaina/Hivisasa.com