Vijana na akina mama katika eneo la Pwani wamehimizwa kujitokeza kwa wingi na kujisajili kama wapiga kura kwenye zoezi litakaloanza rasmi tahehe 15 mwezi huu kote nchini.
Akizungumza na wanahabari huko Changamwe mjini Mombasa baada ya kukamilika kwa kongamano la kuzindua kampeni ya kuwahamasisha wakenya kuhusu kujiandikisha kama wapiga kura, Kamishina wa Tume ya uchaguzi na mipaka Mohammed Alawi alisema kuwa tume hiyo inalenga zaidi vijana na akina mama waliyo na vitambulisho.
Aidha, Alawi amesema kuwa tume hiyo pia inawalenga zaidi wale waliyokosa nafasi ya kujisajili kwenye zoezi la usajili lililofanyika hapo awali pamoja na wanaotaka kubadili vituo vyao vya upigaji kura.
"Kama tume tunalenga sana vijana na akina mama katika kampeni hii ya kuhamasisha jamii ili kuona kwamba usajili wa kura unaongezeka na kufikia milioni 18 kama tunavyotarajia," alisema Alawi.
Wakati uo huo, Alawi ameahidi kushirikiana na idara ya usalama katika kutoa habari muhimu kuhusu watu wanaolenga kuzua vurugu na kuharibu zoezi hilo, huku akilitaja eneo la Lamu kama linakumbwa na changamoto hizo.
Tume hiyo inalenga kusajili wapiga kura milioni 18 na ziadi licha ya kusajili wapiga kura milioni 14.3 katika usajili uliyofanyika mwaka wa 2012 kabla ya uchaguzi mkuu wa mwaka wa 2013.