Vijana katika Kaunti ya Kisii wamehimizwa kutotegemea kazi za ajira, ila kutafuta jinsi ya kupata riziki ya kila siku kwa kujihusisha na biashara.
Akizungumza na mwandishi huyu wa habari siku ya Ijumaa, kiongozi wa vijana katika wadi ya Marani David Omwancha aliwaonya vijana kutotegemea kazi za ajira katika serikali, na kuwahimiza kufanya biashara ili kujiendeleza.
Aidha, aliwaomba vijana kujisirikisha kwa maswala ya biashara, na kutoitikia kutumiwa na wanasiasa kwa kusema wanasiasa wanapofaulu huwasahau baada ya kupata uongozi.
Kulingana na kiongozi huyo, wengi wa wanasiasa wamekuwa wakitumia vijana kubuni ushindi katika uchaguzi wa uongozi, na wengi wao wanapopatika huwasahau vijana.
“Kila kijana katika wadi hii ya Marani na katika kaunti yetu nzima ya Kisii, naomba tushikane pamoja tusimame kidete ili tusitumiwe na wanasiasa, wakati umefika wa kuona ni lipi la kufanya likiwemo nzuri na baya,” alisema Omwancha.
Omwancha aliomba kila kijana aliyefikisha umri wa miaka 18 kuchukua kitambulisho na kadi ya kura ili kubadilisha uongozi wa nchi, huku wakisema uongozi ujao utakuwa uongozi wa kuwakumbuka vijana katika maendeleo.
“Ifikapo mwaka wa 2017, naomba tubadilishe uongozi nchini maana uongozi uliopo kwa sasa haunufaishi vijana, kila kijana awe na silaha yake ambayo ni kitambulisho na kadi ya kura,” aliongeza Omwancha.
Aidha, kiongozi huyo aliomba viongozi walio mamlakani kujaribu kila wawezalo kuwasaidia vijana ili wajiendeleze, la sivyo wakabiliwe vikali ifikapo 2017 wakati wa uchaguzi mkuu.
Kwa sasa kiongozi huyo amewaomba viongozi wa Kaunti ya Kisii kubuni miradi kwa vijana ili nao wawe wanapata zao lao la kila siku.