Vijana katika eneo la Likoni, Kisauni na Jomvu mjini Mombasa wameshinikizwa kujitokeza na kuzuru vituo vya afya kupima hali zao ili kujitenga na maambukizi ya virusi vya Ukimwi.
Shirika moja la kijamii la ‘Jamii imara’ lilisema kwamba vijana wengi hujihusisha na ngono za kiholela bila ya kutumia kinga kutokana na kutolichukulia kwa umuhimu swala la kuzuru vituo vya afya.
Akizungumza katika eneo hilo la Likoni mjini Mombasa siku ya Alhamisi, Afisa mkuu wa Shirika hilo Joy Rui alisema kwamba eneo la Likoni sawa na sehemu nyingine katika kaunti ya Mombasa zinakabiliwa na maambukizi ya virusi vya Ukimwi kutokana na starahe nyingi vijana wanazojihusisha nazo.
“Tumeona idadi ya maambukizi ya virusi vya ukimwi mjini Mombasa kutokana na vijana wengi kutolichukulia kwa umuhimu swala la kuzuru katika vituo vya afya na kutambua hali zao za kiafya, hali ambayo inakuwa vigumu kwa vijana kujiepusha na maambukizi hayo,” alisema Rui.
Rui aliongeza kwamba njia ya kipekee ya jamii kujitenga na maradhi hayo ni kutumia kinga, na zaidi kuzuru vituo hivyo ili kuzuia hali zao za virusi na wabadili mkondo wao wa maisha.
Shirika hilo limesema kwamba litaendeleza hamasa mashinani na kuwalenga zaidi vijana ili kuona kwamba vijana wanajitenga na ngono hizo za kiholela ambazo zimepelekea maambukizi ya virusi.