Share news tips with us here at Hivisasa

Vijana katika eneo la Pwani wameshinikizwa kujitokeza na kuvitembelea vituo vya afya kupimwa hali zao ili kujitenga na maambukizi ya maradhi.

Shirika la kijamii la ‘Jamii imara’, katika eneo la Pwani limesema kuwa kutokana na vijana wengi kutozingatia ushauri kutoka kwa maafisa wa afya na jamii, vijana wengi wamejikuta katika hali ya kujihusisha na ngono za kiholela bila ya kutumia kinga.

Amesema kuwa hali hiyo ni hatari mno hasa kwa kizazi cha sasa na shirika hilo likapendekeza vijana hao kuchukulia kwa umuhimu na umakini suala la kuzuru katika vituo vya afya kujua hali zao na jinsi ya kujikinga kupata maradhi.

Akizungumza katika kongamano la vijana la hamasa Mombasa siku ya Ijumaa, Afisa mkuu wa Shirika hilo Joy Rui amesema kuwa baadhi ya maeneo katika ukanda wa Pwani yanakabiliwa na idadi kubwa ya vijana waliyoathirika na virusi vya ukimwi pamoja na madhara mengine ya kiafya.

“Idadi ya maambukizi ya virusi vya ukimwi mjini Mombasa inazidi kuongezeka kila uchao kutokana na vijana kutolichukulia kwa umuhimu suala la kuzuru katika vituo vya afya na kupata ushauri bora wa jinsi ya kujiepusha na maradhi mbalimbali hatari,” alisema Joy.

Shirika hilo la ‘Jamii imara’ limesema kwamba litaendeleza hamasa mashinani na kuwalenga zaidi vijana ili kuona kwamba vijana wanajitenga na ngono hizo za kiholela ambazo zimepelekea maambukizi ya virusi vya ukimwi.