Share news tips with us here at Hivisasa

Vijana ambao hawajafikisha umri wa kuendesha magari barabarani wameonywa vikali, na wazazi wao kuombwa kuwa makini na watoto wao na kuwaepusha kuendesha magari yao hasa nyakati hizi za sherehe kuelekea krismasi na tafrija za mwaka mpya.

Akiongea na mwandishi huyu siku ya Jumapili jijini Mombasa baada ya ajali mbaya kufanyika na kumwacha mahututi mwendeshaji mkokoteni, afisa msimasi wa trafiki katika eneo la katikati la mji huo, Musa Nasibu alisema kuwa ni kinyume na sheria vijana, hasa watoto ambao hawajafikisha umri wa kujisajili kupata vitambulisho kuendesha magari bila kuwa na uzoevu na vibali rasmi vya kuwaruhusu kufanya hivyo.

Afisa huyo alishtumu ajali hiyo iliyotokea siku ya Jumapili, na kusema imesababishwa na kijana wa chini ya miaka kumi na minane, ambapo aliwalimbikizia lawama nyingi wazazi ambao alisema wamekosa kuwajibikia majukumu ya kuwaongoza watoto wao vizuri.

Alisema kuwa baadhi ya vijana wanaendesha magari ya wazazi wao kwa ufahamu wa wazazi wenyewe, na kuonya kuwa iwapo mtindo huo utaendelea, huenda watoto wengi wakajipata kwenye mkono mbaya wa sheria.

Kulingana na Musa, ajali hiyo ilisababishwa na huendeshaji kiholela wa gari dogo ambalo lilikuwa linatoka eneo la Likoni, ambapo lilimgonga mwanaume mwenye umri wa makamo ambaye hushughulika na biashara ya kuuza madafu kwa mkokoteni.

Mwanamme huyo alipelekwa katika hospitali kuu ya Makadara kupata huduma za matibabu.