Share news tips with us here at Hivisasa

Wazazi wa watoto watano waliofariki kwenye ajali ya barabarani eneo la Salgaa mkesha wa mwaka mpya wamekosoa utepetevu wa maafisa wa polisi, wakihoji mbona hawakuwa barabarani usiku huo wakifanya doria.

Wakiongea na wanahabari katika eneo la Njoro Kaunti ya Nakuru, wazazi hao walisema wanao hawakuwa na leseni za uendeshaji magari, hivyo basi kama polisi wangekuwa na kizuizi kwenye barabara hiyo ya Nakuru-Eldoret, wangefaulu kuzuilia vijana hao.

Hata hivyo Peter Chege, babake Kelvin Chege, mmoja kati ya watano hao, alisema kwamba mwanae alikua amepitia mafunzo ya uendeshaji magari, lakini hakuwa amepata leseni. 

Wazazi hao pia waliitaka serikali kuchunguza madai kwamba gari ambalo vijana hao wanane walikuwa nalo wakati wa mkasa huo katika eneo la Teachers, linamilikiwa na afisa mmoja wa polisi.

Mmoja wa wazazi hao alikemea watu wanaopika na kuuzia vijana pombe, akisema wanaharibu kizazi cha sasa.

Vijana watatu waliepuka na majeraha madogo kwenye mkasa huo wa saa nane mkesha wa mwaka mpya, uliohusisha gari ndogo na basi la usafiri la Mbukinya.