Share news tips with us here at Hivisasa

Chifu wa eneo la Langalanga viungani mwa mji wa Nakuru George Ng’ang’a amekanusha madai yaliyotolewa na baadhi ya vyombo vya habari kuwa vijana waliokuwa wakizozana hivi maajuzi katika eneo la Kivumbini ni wa kundi haramu la Mungiki.

Akizungumza siku ya Jumanne katika maadhimisho ya siku ya akina mama duniani yaliyofanyika katika ukumbi wa rumande ya watoto huko Bondeni, chifu huyo alisema kuwa washukiwa wawili waliotiwa mbaroni walikuwa wa kutoka jamii ya Luhya na Luo.

“Kuna wakati vyombo vya habari vilikuwa vimeripoti ati kuna kundi la Mungiki. Vijana hao hawakuwa wa kundi hilo. Hayo yalikuwa tu makundi ya vijana kutoka Rhonda yaliyokuwa yakipigana,” alisema Ng’ang’a.

Aidha, aliwahakikishia wakaazi wa eneo la Kivumbuni usalama wao kwa kusema kuwa maafisa wa polisi wanaendeleza doria katika eneo hilo.

“Nataka kuwahakikishia usalama wenu. Hao watu waliokamatwa Jumatatu na Alhamisi hakuwa kundi la Mungiki kwani mmoja wa aliyeshikwa alikuwa kutoka Jamii ya Luhya na mwingine kutoka Jamii ya Luo,” alisema Ng’ang’a.

Wakati huo huo, amewataka wakaazi wa Nakuru kupiga simu kwa nambari ya 0736 350 372 kutoa ripoti kuhusu tukio lolote la uhalifu.

Inadaiwa kuwa genge kutoka mtaa wa Flamingo kwa jina la 'Confirmed' lilivamia genge la 'Dragon' kutoka Rhonda, ili kulipiza kisasi kufuatia mashambulizi ya vijana wawili wa umri wa miaka 16 na 17 wiki jana.