Share news tips with us here at Hivisasa

Vijana kutoka Kaunti ya Mombasa wanamtaka rais Uhuru Kenyatta kuanzisha mfumo wa vijana ‘Political Mentorship’ katika kila Kaunti ili kuwapa vijana mwongozo mwema ya jinsi ya kufanya masuala ya kisiasa katika viwango mbali mbali vya kaunti na taifa.

Vijana hao, wakiongozwa na Andrew Mwasia, kutoka eneo bunge la Jomvu, katika mkutano ambao uliandaliwa katika ikulu ya rais huko Mombasa siku ya Jumatano walisema kuwa wengi wa wanasiasa katika eneo la Pwani na Kenya kwa jumla wana mtindo mmoja wa kuwatumia vijana katika masuala ambayo yanawahusu na nyakati za kutafuta kura tu.

Aidha, vijana hao wamemtaka rais kuhakikisha kuwa kunaanzishwa wakfu wa kuwatambua vijana ambao wamekuwa mashujaa kwa kufanya na kutekeleza masuala flani ya kitaifa kwa ushupavu kutambuliwa rasmi kila siku kuu za kitaifa kwa kupewa hati rasmi.

Kwa upande wake, Rais Kenyatta, ambaye alikuwa anajibisha na kuyajibu maswali ambayo yaliulizwa moja kwa moja kwenye mkutano huo aliwahakikishia vijana wote ambao walihudhuria kuwa maombi yote waliwasilishwa yatazingatiwa na kutekelezwa mara moja.

Mkutano huo ulihudhuriwa na vijana mbali mbali kutoka kaunti tofauti za eneo la Pwani ambao walipata nafasi hiyo adhimu na kutoa mitazamo yao mbele ya rais.