Vijana wanaojihusisha na wizi wa mifugo katika wadi ya Gesima, kaunti ya Nyamira wameombwa kujisalimisha kwa maafisa wa polisi kabla ya kuchukuliwa hatua.
Akihutubu katika eneo hilo siku ya Alhamisi alipofanya mkao na wazee wa vijiji, naibu chifu kwenye kata ndogo ya Riamoni Sambu Bosire alisema kuwa alilazimika kuongeza muda wa makataa ili wahusika wengine waliotajwa na vijana waliojisalimisha waweze kujisalimisha kwa maafisa wa polisi kabla ya hatua kuchukuliwa dhidi yao.
"Nimeshauriana na wazee wa vijiji na tumekubaliana kuongeza muda zaidi kwa vijana waliotajwa na wale tayari wamejisalimisha waweze kujiwasilisha kwa hiari kwa maafisa wa polisi kabla ya sisi kuamua kuchukua hatua dhidi yao," alionya Bosire.
Chifu huyo aidha alisema kuwa kamwe utawala wake hautasita kuweka mikakati ya kuhakikisha kuwa visa vya wizi wa mifugo vinakabiliwa vikali, huku akiongeza kuwasihi wazazi ambao wanao walitajwa kama washukiwa wa wizi wa mifugo kuwarahi wanao kuepukana na tabia hiyo kabla ya serikali kulazimika kuwachukulia hatua kali.
"Tabia ya wizi wa mifugo ni mojawapo ya tabia ambazo zimepitwa na wakati na kamwe hatutaruhusu tabia hiyo kuendelea hapa na ninawaomba wazazi ambao wanao wamehusishwa pakubwa na madai ya kuhusika na wizi wa mifugo kuwarahi wanao kuasi tabia hiyo kabla ya serikali kuwachukulia hatua kali," alisisitiza Sambu.