Vijana wa kaunti ya Nyamira wamepewa changamoto ya kupata mafunzo maalum yatakayowawezesha kupigana na ukosefu wa kazi miongoni mwao.
Akihutubia kikundi cha vijana siku ya Jumapili kule Kebirigo, waziri wa masuala ya Jinsia, Vijana, Spoti na utamaduni Peter Ogwara alisema kwamba kaunti ya Nyamira ina vijana wengi waliosomea taaluma mbalimbali, lakini wanategemea kuajiriwa badala yakujiajiri wenyewe.
“Kaunti ya Nyamira ina vijana wengi ambao wamesomea taaluma mbalimbali, ila hawana kazi kwa kutegemea kuajiriwa, na ningependa kuwasihi wabuni kazi badala ya kungoja kuajiriwa,” alisema Ogwara.
Waziri Ogwara aliongeza kwa kusema kuwa idadi ya vijana wasio na ajira inazidi kuongezeka nchini, huku akiwahimiza vijana kujiunga kwenye makundi ili kujisajili kupokea mikopo kutoka kwa serikali ili waanzishe biashara mbalimbali.
“Idadi ya vijana wanaokosa ajira humu nchini inaendelea kuongezeka, na ningependa kuwahimiza vijana wajiunge kwenye makundi na kujisajili kupokea mikopo kutoka kwa serikali ya kaunti na ile ya kitaifa ili waanzishe biashara zao,” alisema Ogwara.
Waziri Ogwara aidha aliongeza kwa kusema kuwa tayari serikali ya kaunti ya Nyamira imetenga pesa za kuwafunza vijana kujitegemea maishani, huku akiwasihi vijana kujiepusha na tabia ya utumizi dawa za kulevya, na badala yake wafanye biashara za kuwaimarisha.
“Serikali ya kaunti hii imetenga pesa za kuwafunza vijana kuhusu ni vipi wanaweza imarisha mbinu zao za kufanya biashara,” alisema Ogwara.