Share news tips with us here at Hivisasa

Kiongozi wa vijana katika eneo bunge la Mugirango Kusini kaunti ya Kisii Geoffrey Mengo amewashauri vijana katika eneo bunge hilo kujiandikisha kupata vitambulisho kwa wingi ili kubadilisha uongozi ifikapo mwaka wa 2017.

Wito huo umetolewa baada ya vijana wa eneo hilo kukiri kuwa wamekuwa wakitengwa na viongozi wa eneo hilo kwa kusahaulika baada ya kuwachagua viongozi.

Akizungumza na waandishi wa habari siku ya Jumapili katika eneo la Etago, Mengo alisema wanasiasa wengi katika kaunti ya Kisii huwatumia vijana kupata kura nyingi, na wanapochaguliwa huwasahau.

Hili alilitaja kama jambo ambalo limewalazimu vijana kuhimiza vijana wengine kujiandikisha kupata vitambulisho na kadi za kura ili kubadilisha uongozi katika uchaguzi ujao.

“Wanasiasa wengi hututumia sisi vijana kama daraja ya kuvuka kwa kupata uongozi, na wanapokabidhiwa mamlaka hayo hutusahau sisi vijana na hawajawahi kutukumbuka kamwe, hata tumeshindwa la kufanya lakini hili liko na suluhu,” alisema Mengo.

“Naomba vijana katika eneo bunge hili letu la Mugirango kusini na hata katika kaunti nzima ya Kisii  ambao wamefikisha miaka 18 kuchukua vitambulisho kwa wingi na kuandikisha kupata kadi za kura ili nasi tuwachague viongozi ambao ni vijana ambao pia watasaidia vijana wengine,” aliongezea.

Aidha, Jane Obae, kijana mwingine alisema idadi nyingi ya vijana waligeukia sekta ya uchukuzi kwa kuendesha bodaboda, lakini jinsi mvua inaendelea kunyesha barabara hazipitiki kwa kile walichokisema kutokarabatiwa kwa barabara na viongozi waliochaguliwa.