Do you have a lead on a newsworthy story? Share news tips with us here at Hivisasa!

Mradi wa vijana unaofadhiliwa na shirika la kitaifa la huduma kwa vijana unapaswa kuwakimu mamia ya vijana katika eneo la Kisauni kama njia moja wapo ya kuwakinga na uhalifu.

Akizungumza katika uwanja wa Tononoka mjini Mombasa wakati wa maadhimisho ya siku kuu ya Jamhuri siku ya Jumamosi, Kamishna wa Kaunti ya Mombasa Nelson Marwa alisema kwamba vijana wengi katika eneo hilo wamejiunga na makundi ya kihalifu.

Aidha alisema kwamba inasikitisha mno kuwaona vijana wadogo wakiwahangisha wakazi katika eneo hilo, na iwapo watasajiliwa katika mpango huo, basi usalama utaimarishwa.

“Tunawaomba vijana kujitenga na uhalifu na kujiunga na NYS kupata mafunzo bora yatakayowasaidia kujikimu kimaisha badala ya kujihusisha na uhalifu kwani maafisa wa usalama watawakabili,” alisema Marwa.

Marwa amesisitiza kwamba oparesheni ya kiusalama dhidi ya makundi ya ‘Wakali wao’ na ‘Wakali kwanza’ itaimarishwa zaidi katika eneo hilo la Kisauni, hususan wakati huu wa msimu wa sherehe za Krismasi.

“Lazima oparesheni ya kuwasaka wahalifu katika eneo la Kisauni kendelezwa hadi pale wahalifu watakapojisalimisha na kuimarisha usalama,” aliongeza Marwa.

Katika kipindi cha majuma mawili yaliyopita, eneo la Kisauni limeshuhudia oparesheni kali ya kiusalama baada ya lalama kutoka kwa wakazi ya kuangaishwa na wahalifu.