Is there a story unfolding in your community? Let Hivisasa know

Wakenya wa tabaka mbali mbali wanapoendelea kuomboleza kifo cha mtangazaji maarufu wa habari za runinga ya KTN Ahmed Darwesh, ambaye alizikwa siku ya Jumanne jijini Mombasa, viongozi mbalimbali waliohudhuria sherehe za kumuaga gwiji huyo wamewataka wakenya wengine hasa wanahabari wanaoinukia kuiga mfano wa mwendazake kwa kuwa wanyenyekevu.

Wakiongozwa na mbunge wa Mvita, Abduswamad Shariff Nassir, ambaye alikuwa miongoni mwa viongozi waliohudhuria mazishi siku ya Jumanne, walimtaja kuwa mtangazaji mwenye taadhima na heshima kwa mtu yeyote bila kujali umri, na kuwataka vijana wanaoinukia kwenye masuala ya uandishi wa habari na hata taaluma nyingine kufuata mienendo ya mtangazaji huyo.

“Darwesh alikuwa mtu wa kutangamana na kila mtu awe mkubwa au mdogo, na alikuwa rafiki yangu mkubwa na tumepoteza mtu wa maana sana katika nchi ya Kenya, na alikuwa mshauri wa watu wengi ambao walitangamana naye,” aliongeza kiongozi huyo.

Miongoni mwa wale waliohudhuria mazishi ni gavana wa Mombasa Hassan Joho, seneta wa Nairobi Mike Mbuvi Sonko, watangazaji wenza wa KTN, pamoja na viongozi wa Kaunti ya Mombasa na wakazi mbali mbali kutoka sehemu zote nchini Kenya.

Darwesh aliaga dunia siku ya Jumatatu jioni baada ya kuugua maradhi ya kisukari kwa muda, na kabla ya kuaga alikuwa amefanya kazi na shirika la utangazaji la taifa la KBC, kwenye redio ya Pwani Fm na runinga ya KBC na baadaye kujiunga na KTN alikokatiziwa taaluma yake na mauti.