Share news tips with us here at Hivisasa

Huku siku kuu ya ukimwi ikisherehekewa siku ya Jumanne, kundi moja la kijamii kutoka wilaya ya Likoni katika Kaunti ya Mombasa limewataka vijana kujitokeza na kupimwa hali yao ili kuepusha uambukizaji zaidi.

Kundi hilo linajihusisha na uhamasisho na utoaji wa ushauri nasaha jinsi ya kuishi vizuri na kujiepusha na maradhi ya ukimwi na kuwashauri wale ambao washaambukizwa jinsi ya kuishi kwa afya nzuri.

Kundi hilo, Jamii Imara, likongozwa na Joy Rui kwenye mahojiano alisema kuwa wengi wa vijana bado hawajaonyesha umuhimu wa kujiwasilisha katika vituo vya kupimwa na kukaguliwa hali zao kwa kuogopa kubaguliwa, na kudai kuwa hata wengine wanahisi kuwa huenda wanapoteza nafasi yao katika jamii iwapo watajipata kuwa wana gonjwa hilo.

“Vijana wengi bado hawana ari, hata hawajaonyesha moyo wa kutaka kujua hali zao kwa sababu ya kuwa na ubaguzi wa hali ya juu miongoni mwa jamii zetu, hivyo basi kuwafanya kutohudhuria katika kupimwa hali zao kwenye vituo husika,” alisema Rui.

Kiongozi huyo aliwataka vijana pamaoja na wale tayari wamepata maradhi hayo kujipa moyo na pia kushiriki katika makundi ya ushauri nasaha ambayo yako takribani kila kata, hasa katika jiji la Mombasa ambalo alisema limebahatika kuwa na mashirika mengi ya kuhamasishana kuhusiana na athari za kutopimwa hali zao kama vijana.