Share news tips with us here at Hivisasa

Mwenyekiti wa chama cha maendeleo ya wanawake mjini Mombasa Afya Rama,amewalaumu viongozi wa kisiasa na hata wa kidini kwa kile amekitaja kama kuchangia vijana wengi kuzidi kuhathirika na matumizi ya mihadarati mkoani humo kwa kukosa kuwapa hamasisho

Akizungumza na wanahabari afisini mwake mjini Mombasa siku ya Jumatano, Rama alisema kuwa kukosekana kwa hamasisho miongoni mwa vijana kumechangia wengi wao kupoteza mwelekeo na matumaini maishani, jambo ambalo limewafanya kuzidi kuzitumia dawa hizo za kulevya.

‘’Tumefeli kama viongozi, hatuwajali vijana wetu licha ya changamoto za kimaisha zinazowakumba. Lazima tuwe katika mstari wa mbele kutoa hamasa kwa vijana ili swala hili la utumiziwa mihadarati liweze kupungua,’’ alisema Afya.

Rama vilevile alisema kuwa chama chao mjini Mombasa, hivi karibuni kitaanza kuzuru mashinani katika jitihada zinazolenga kuwafikia vijana walioathiriki na dawa za hizo ili kuwapa mafunzo kuhusu namna wanavyoweza kujikwamua kutoka katika shida hiyo.

Aidha, aliwasuta viongozi wa kisiasa mjini humo wanaowatumia vijana kuzua vurugu, na kuwataja kama wanaoyajali maslahi yao ya kibinafsi badala ya wananchi waliowachagua.