Share news tips with us here at Hivisasa

Viongozi wa makanisa pamoja na serikali ya kaunti ya Kwale waliandaa kongamano la pamoja kujadili kwa kina swala la itikadi kali miongoni mwa vijana, linalosumbua kaunti hiyo pamoja na ukanda wa Pwani kwa jumla.

Katika kongamano hilo lililofanyika katika hoteli moja huko Diani siku ya Jumatatu, viongozi hao waliahidi kwa pamoja kushirikiana kukabili changamoto hiyo.

Akiongea katika kongamano hilo, mkuu wa idara ya elimu katika kaunti ya Kwale Mangale Munga alisema kuwa kanisa lina jukumu kubwa katika kuwahamasisha vijana.

“Tumeona kwamba kanisa liko na jukumu muhimu kuhakikisha kwamba hili tatizo la itikadi kali linakomeshwa, kwa sababu watu wanaoathirika zaidi ni vijana wetu na jamii kwa pamoja,” alisema Mangale.

Aidha, viongozi hao pia walikubaliana kupeleka kampeni hiyo hadi mashuleni ili kuwahamasisha wanafunzi dhidi ya janga hilo linalohofiwa kuleta utengano mkumbwa miongoni mwa jamii zinazoishi eneo la Pwani.

Vijana katika eneo la Pwani wamekuwa wakilaumiwa kutokana na kile serikali imekuwa ikitaja kama itikadi potovu zinazoendeshwa na baadhi ya viongozi wa kidini.

Mamia ya vijana wamewahi kukamatwa miaka ya 2014 na 2015 wakihusishwa na shughuli hizo.

Baadhi yao wamekuwa wakishukiwa na idara ya usalama kuwa wanaendelea na harakati za kujiunga na makundi haramu ya kigaidi.

Viongozi mbalimbali wa kidini ikiwa ni pamoja na waislamu na wale wa kikristo wameonekana kuungana pamoja kuubiri amani na kuhamasisha vijana kuhusu swala hili.