Viongozi wa wa dini ya Kiislamu nchini wamehimiza serikali kutoyaondoa majeshi ya Kenya nchini Somalia licha ya baadhi ya viongozi wa kisiasa kupendekeza wanajeshi hao kusitisha vita dhidi ya wanamgambo wa Al Shabaab.
Wakiongozwa na mkurugenzi mkuu wa baraza la maimam nchini (SUPKEM) Hussein Omar, viongozi hao wamesema kuwaondoa wanajeshi wa Kenya nchini Somalia kutawapa nguvu wanamgambo wa Al Shabaab na kuhatarisha usalama wa nchi.
''Tunaiunga mkono serikali katika vita dhidi ya Al Shabaab na tunahimiza isilegeze kamba kwani ndiyo njia ya pekee ya kuilinda nchi yetu dhidi ya magaidi,'' alisema Omar.
Viongozi hao walikuwa wakizungumza mjini Eldoret siku ya Jumamosi ambapo pia waliwaombea familia ambazo zilipoteza jamaa yao katika shambulizi lililotekelezwa na wapiganaji wa Al Shabaab siku ya Ijumaa katika eneo la El-Ade nchini Somalia.
Kauli yao inajiri wakati baadhi ya viongozi nchini akiwemo kinara wa upinzani Raila Odinga, wakizidi kuishinikiza serikali kuyaondoa majeshi ya Kenya nchini Somalia kwa dai kuwa ndiyo hatua itakayolikomesha shambulizi la mara kwa mara linalotekelezwa na magaidi nchini.