Viongozi wa mrengo wa Jubilee nchini wameahidi kuwasilisha mswada bungeni wa kujadili maswala muhimu ya kuimarisha shughuli za taifa hili kutokana na madai kwamba serikali imeshindwa kuwajibikia majukumu yake.
Akiongea na wanahabari mjini Mombasa siku ya Jumatato baada ya mkutano wa faraga, wabunge hao wakiongozwa na Mithika Linturi walisema kwamba serikali ina kumbwa na changamoto za kiuchumi kutokana na kukithiri kwa kashfa za ufisadi.
Linturi alisema kwamba serikali inagharamika zaidi kulipa viongozi wa umma ambao walibanduliwa mamlakani kutokana na kashfa za ufisadi, swala ambalo linastahili kushughulikia mara moja na iwapo viongozi hao wana hatia, basi wafutwe kazi.
Linturi, aliongeza kusema kuwa muungano huo uko tayari kufanya mazungumza na rais Uhuru Kenyatta ili kuona kwamba taifa hili linaimarika kiuchumi, huku akiwashinikiza viongozi kujitenga na ufisadi.
"Tuko tayari kuwasilisha mswada bungeni kujadili maswala mihimu ya kuimarisha taifa hili, ili kuona kwamba tunasaidia uchumi wetu na pia tutafanya mazungumzo na rais kuhusu maswala haya," alisema Linturi.
Mapendekezo ya viongozi hao yamejiri baada ya serikali kukumbwa na changamoto za kiuchumi zinakisiwa kuchangiwa na kukithiri kwa kashfa za ufisadi nchini.