Viongozi wa kidini na wale wa serikali pamoja na wanasiasa wamehimizwa wajitokeze katika makabiliano dhidi ya misimamo mikali miongoni mwa vijana katika Kaunti ya Mombasa.
Hayo yamedokezwa na afisa mkuu wa shirika la Kijamii la ‘Kenya Community Support Centre’ Bi Phyllis Muema.
Akizungumza Mjini Mombasa Jumatano, Muema alisema kwamba japo hapo awali pande zote mbili zilijitenga na swala hilo na kuliwachia jukumu hilo Mashirika ya Kijamii na yale ya utetezi wa haki za kibinadamu, alisema kwamba viongozi hao wana jukumu kubwa katika kulitatua tatizo hilo.
Muema aliongeza kwamba tatizo hilo, japo ni la kiusalama ni la kijamii vile vile, na iwapo viongozi wa kidini, wale wa kisiasa, viongozi serikalini na jamii yenyewe hawatashirikiana kulitanzua, basi tatizo la itikadi kali miongoni mwa vijana wa Pwani litakithiri.
“Janga hili linahitaji ushirikiano kutoka kila upande, la sivyo, vijana wengi watasajiliwa katika makundi ya kigaidi na kutishia usalama wa nchi, hususan wa eneo la Pwani,” alisema mwanaharakati huyo.
Hata hivyo, Muema alisema kwamba kwa kiwango kikubwa, juhudi za shirika hilo za kuwahamasisha vijana kuasi itikadi kali kupitia kwa mradi wake wa ‘Kataa kutumiwa’ umefaulu, japo unahitaji kuungwa mkono zaidi na jamii, viongozi sambamba na maafisa wa usalama ili uafikie malengo yake ya kuwakinga vijana dhidi ya janga hilo.
Harakati hizo za kuwahamasisha vijana kuhusu athari za kujiunga na makundi ya kigaidi na kuwa na itikadi kali zinaendelezwa kote Pwani katika juhudi za kuwalinda vijana dhidi ya misimamo mikali.
Kulingana na takwimu za idara ya polisi nchini, zaidi ya vijana 10,000 kutoka eneo la Pwani wamesajiliwa na makundi ya kigaidi tangu mwaka wa 2011.