Is there a story unfolding in your community? Let Hivisasa know

Viongozi wa kidini humu nchini wameombwa kuja pamoja na kutafuta mbinu za kuwasaidia wasichana na wanawake ambao wamekwama katika jinamizi la ukahaba hapa nchini.

Mbunge wa eneo bunge la Nakuru mashariki David Gikaria amesisitiza kuwa viongozi hao wa kidini wakijitolea na kujitokeza kuwasaidia wanawake hao wanaodaiwa kuwa makahaba itachangia asilimia kubwa katika kubadili mienendo katika jamii humu nchini.

Akizungumza na waandishi wa habari hapa mjini Nakuru Jumamosi, Gikaria aliongeza kuwa ni makosa kwa viongozi wa kidini kulifumbia macho swala hilo, huku uozo ukizidi kukita mizizi katika jamii.

Gikaria, ambaye ni mwanachama katika kamati ya bunge kuhusu usalama humu nchini amesema kuwa serikali iko tayari kushirikiana na viongozi hao wa kidini ili kujaribu kukomesha uozo huo, jambo ambalo amesema litasaidia serikali katikia kuokoa raslimali nyingi ili kukabiliana na visa vya uhalifu hapa nchini.

Gikaria ambaye ameweka bayana kuwa yeye ni mkatoliki na mfuasi sugu wa dini hiyo amewaomba maaskofu, makasisi, mapadre, waumini mbalimbali pamoja na viongozi wengine wa dini mbalimbali humu nchini kuungana pamoja na kuwasaidia akina dada hao, badala ya kuwakemea, kuwatusi na hata kuendeleza unyanyapaa dhidi yao.