Baraza la Maimam na wahubiri kanda ya North Rift limejiunga na baadhi ya viongozi nchini ambao wanamtaka Rais Uhuru Kenyatta kuvunjilia mbali baraza la mawaziri.
Baraza hilo limesema kuvunjiliwa mbali kwa baraza la mawaziri ni njia moja ya kukabiliana na ufisadi ambao unadaiwa kukita mizizi katika wizara mbalimbali.
Mwenyekiti wa baraza hilo Sheikh Abubakar Bin alisema mbali na kuvunjiliwa mbali kwa baraza hilo kuna haja ya kufanyika kwa kura ya maamuzi ili kufanyia katiba marekebisho.
Sheikh Bin alidai kuwa aslimia kubwa ya changamoto ambayo inakumba nchi hii kwa sasa inatokana na vipengele fulani vya katiba.
Akihutubu mjini Eldoret Jumatatu hii Sheikh Bin alisema uongozi bora utaafikiwa kupitia kwa marekebisho katika katiba ya mwaka 2010.
Akirejelea madai ya kuwepo kwa ufisadi katika wizara ya ugatuzi Sheikh Bin alisema njia ya pekee ya kukabiliana na sakata kama hiyo ni kufanyia baraza lote la mawaziri mageuzi ya kina.
Kulingana na Sheikh Bin ni kwamba itakuwa bora zaidi kwa waziri wa ugatuzi Anne Waiguru kujiuzulu hata kabla ya baraza husika kufanyiwa marekebisho.
“Kume kuwa na kashfa nyingi za ufisadi nchini ufisadi umeonekana kukita mizizi katika kila wizara,ni sharti baraza lote la mawaziri livunjiliwe mbali ili kumaliza ufisadi” alisema Sheikh Bin
Msimamo wa Bin umeungwa mkono na mlezi wa muungano wa Jubilee North-Rift Joseph Wainaina ambaye amesema madai ya ufisadi katika wizara ya ugatuzi yanapaka tope utawala wa Jubilee.
“Kile ambacho nashauri rais ni kufanyia marekebisho baraza lote la mawaziri, mahala ambapo madai ya ufisadi katika wizara ya ugatuzi yamefikia ni fedheha kubwa kwa serikali” alisema
Wainaina ambaye ni mwandani wa rais alitaka upinzani kutotumia madai ya ufisadi nchini kujinufaisha kisiasa.
Kiongozi huyo alitoa changamoto kwa upinzani kushauriana na rais kuhusu njia bora za kuboresha maisha ya Wakenya wa matabaka yote.
“Nchi ya Kenya ni zaidi ya upinzani tunataka upinzani kuondoa ubinafsi katika swala hili na kushauriana na serikali kuhusu njia bora za kuboresha maisha ya Wakenya wote” alisema Bw Wainaina