Baadhi ya wanasiasa kutoka Nyamira wameishtumu vikali serikali ya Jubilee kwa kutochukua hatua ya kuhakikisha kwamba wakimbizi wa ndani kwa ndani wametengewa sehemu za kuishi ili kurejelea maisha yao ya kawaida.
Akihutubu kwenye hafla ya mazishi kule Borabu siku ya Jumatatu, wakili Omogeni alishtumu vikali serikali hiyo kwa kutosuluhisha suala hilo la wakimbizi, huku akionya kuwa kamwe Jubilee isiwahuzishe watu ya jamii ya Abagusii kwenye siasa zao iwapo matakwa ya wakimbizi hao hayatoafikiwa, akiongezea kwa kuwahimiza wakazi kuupigia mlengo wa Cord kura kwenye uchaguzi mkuu ujao.
"Kuna ndugu zetu wanaoendelea kuteseka kwenye kambi kwa sababu kuwa serikali ya kitaifa haijawafidia na tunafahamu kwamba baadhi ya wakimbizi kutoka maeneo mengine tayari wamefidiwa, huku wale wa maeneo ya Gusii wakiendelea kuhangaika na iwapo serikali haitochukua hatua ya kushughulikia matakwa yao wacha wabaki wakijua kwamba kamwe sisi Abagusii hatutawapigia kura," alionya Omogeni.
Kwa upande wake seneta wa Kaunti ya Nyamira Okongo Mong'are aliipa wizara ya ugatuzi makataa ya wiki mbili kuweka bayana ripoti ya wakimbizi ambao tayari wamefidiwa na wale ambao wangali kufidiwa kabla yake kuwasilisha suala hilo kwenye bunge la seneti.
"Sharti wizara ya ugatuzi ijitokeze bayana kuwaelezea wakenya idadi kamili ya wakimbizi ambao tayari wamefidiwa kwa maana hatuwezi keti huku ndugu zetu wengine wanaostahili kufidiwa na serikali wakiendelea kuteseka na kamwe hilo halitaruhusiwa," alisema Mongare.